Na; Frt
Peter Mwikwabe
“Utusamehe makosa yetu kama
tunavyowasamehe na sisi waliotukosea”
[Mathayo 6:12]
Msamaha ni hali ya kuachilia
maumizo na makwazo uliyotendewa na kuacha moyo wako kuwa huru na kusahau
yaliyopita. Msamaha ni kanuni ya maisha, Mungu alipotuumba katika ubinadamu
wetu alituwekea kanuni ya lazima yaani kusamehe. Matokeo ya kushindwa kuifuata
kanuni hii ni kutosamehe ambako kunatutesa tulio wengi. Msamaha ni hitaji lililositizwa
kwa kiasi kikubwa katika neno la Mungu, soma vifungu vifuatavyo, Kolos 3:8-9, Mt 18;21-34, Mk 14;66-72, Efe 4;31-32,
Mt 6;15, Lk 6;36, Mt 5;23-24, Rum 12;17-21, Ebr 8;12, Luk 6:27-28, 1Sam 25:1-37,
Mdo 6;8-10, 7;54-60, Zab 51:1-19, Mith 19;11, Sira 28;1-3, Law 19;17-18, Luka
23;34.
Swali. Je, tunaweza kusamehe na kusahau
?Jibu nindiyo, ni kweli wanadamu tumepewa uwezo wa kukumbuka tena mambo
mengi tu. Tunaposema kusamehe na kusahau maana yake ni kwamba, ukishamsamehe
mtu aliyekuumiza hata kama utaendelea kukumbuka na kuhisi kinyongounapaswa
kuachia maumizo yote na usiendelee kuliongelea jambo lililokuumiza, kwani
kufanya hivyo ni kutonesha kidonda. Kumbukumbu za maumivu zitakuwepo kwa sababu
ni ubinadamu lakini jiachie kwa Bwana Yesu atakusaidia na taratibu utasahau,
lakini usimwambie mtu nimekusamehe lakini sitakusahau, hapo utakuwa bado
haujaanza mchakato wa kusamehe. Unaposamehe na kusahau unafungua ukurasa mpya
wa maisha na hakuna kurudi nyuma, ni kama vile ukishatapika hakuna kuyarudia
yale matapishi huko ndiko kusamehe na kusahau.
Msamaha unaponya, Daktari Louis
Hay katika kitbu chake cha You can heal your
life [unaweza kuponya maisha yako] anasema kuwa, asilimia kubwa ya magonjwa ya
binadamu yanatokana na hali yetu ya kushindwa kusamehe. Ni kweli kabisa
magonjwa mengi tuliyonayo binadamu ni kwa sababu ya kushindwa kusamehe.
Tukumbuke kuwa unaposhindwa kufungua moyo na kusamehe unatengeneza sumu mwilini
mwako bila wewe kujua, kwa watu wengi wanaotawaliwa na hasira huwa
wanajipungizia muda wa kuishi, wataaalamu wa afya wanasema kuwa unapokasirika
mwili unatumia nguvu nyingi ambazo zilibidi zitumike kwa ajili ya kusukuma
damu, kufanya mmeng’enyo wa chakula na kuendesha mifumo mingine ya kimwili.
Unapokasirika unavuruga mifumo hiyo inayoongoza mwilina hivyo kujisababishia
maradhi kama ya kansa, vidonda vya tumbo, maumivu ya uti wa mgongo, presha,
kisukari, TB nk. Ili kuthibitisha hili mwaka 2009 wataalamu wa afya kule
Bangalore nchini India walifanya utafiti na kusema kuwa, kwa wagonjwa wengi
maumivu makali ya uti wa mgongo hutokana na hali ya kushindwa kusamehe.
AINA ZA MSAMAHA
Msamahaumegawanyika katika makundi
makuu manne yote yana lengo la kuleta
Amani na uponyaji.
(a)
Kujisamehe
mwenyewe
(b)
Kumsamehe
Mungu
(c)
Kusamehe
tetesi
(d)
Kusamehe
wengine
Kujisamehe mwenyewe
Katika kuanza mchakato wa
kusamehe ni vema kwanza kutambaua umuhimu wa kujisamehe, yaani kujifariji,
kujiwazia mawazo mazuri, kujipenda na kujithamini. Wengi tunashindwa kusamehe
kwa sababu bado hatujajisamehe tumebeba majeraha moyoni na wala hatujiwazii
mawazo mema. Unapojisamehe unamuweka huru mfungwa, na utagundua kuwa mfungwa
ulikuwa wewe mwenyewe ndani ya gereza la moyo wako. Mungu mwenyewe anasema,nimekupenda
kwa upendo wa milele ndio maana nimekuvuta kwa fadhili zangu [ Yer 31:3],
kwa hiyo una kila sababu ya kujjipenda na kujisamehe kwa sababu hata Mungu
anakupenda kuliko unavyofikiri, sikiliza anavyosema kupitia neno lake
Je, mwanamke anaweza kumsahau
mtoto wake anyonyaye.
Hata asimhurumie mwana wa tumbo
lake?
Naam hawa waweza kusahau,
Lakini mimi sitakusahau wewe.
Tazama nimekuchora kwenye viganja
vya mikono yangu,
Kuta zako ziko mbele yangu daima.
[ Isaya 49:15-16]
Utafiti uliofanywa na chuo kikuu
cha Havard Marekani ulitoa ujumbe huu, ukitaka kuwa na Afya njema, kuishi muda
mrefu pasipo msongo wa mawazo na mfadhaiko ni lazima kujenga utamaduni wa
kuachilia maumivu ya zamani na kusamehe.
Msamehe Mungu
Wakati mwingine Mungu huamua
kutupitisha katika changamoto na magumu mbalimbali ya maisha kwa mfano Ayubu. Lengo
la kufanya hivi ni kuimarisha Imani yetu hata Bwana Yesu alipitishwa kwenye
mateso. Nyakati kama hizi tunapaswa kuwa wanyenyekevu na kupokea mapenzi ya
Mungu kwa moyo mkunjufu, kwa mfano mama Hellen Keller aliyekuwa mwandishi wa
vitabu vya kutia moyo na kuleta matumaini huko nchini Marekani, alipatwa na
matatizo makubwa ya kiafya hali iliyompelekea kupoteza uwezo wa kusikia lakini
yeye alimsamehe Mungu kwa kuyapokea mateso kwa moyo mkunjufu, hata alipoulizwa
ungependa Mungu akutendee nini, yeye alijibu ningepenada Mungu atujalie sisi
sote kuishi kwa Amani, Tumsamehe Mungu kwa kuruhusu mateso yatupate [Ebr
12:4-7]. Ayubu pia alimsamehe Mungu kwa kuyapokea mateso yake kwa moyo wa
matumaini, Ayubu alisema ikiwa tumepokea mema toka kwa Mungu kwa nini
tusipokee na mabaya. Ayubu aliendelea kuweka matumaini yake kwa Mungu lakini
yeye aijua njia niendeayo, akisha kunijaribu nitatoka kama dhahabu [Ayub 23;10]
Kusamehe tetesi zote
Maishani tunakumbana na tetesi na
maneno mengi, mengine ya kukatisha tamaa na kuvunja mioyo, samehe tetesi zote,
samehe maneno yote mabaya yaliyonenwa juu yako, samehe maneno ya chuki, dharau
na kejeli yaliyosemwa dhidi yako. Mtazame Yesu kristu aliyesemwa vibaya na
kutukanwakila aina ya matusi lakini alisamehe
na wala hakukata tamaa. Yesu kristu aliitwa mlafi na mlevi [Luka 7:34],
aliitwa mwendawazimu [Marko 3:21], aliitwa mkiuka mila [Luka 11;45], aliitwa
mtoa maneno ya kufuru [Luka 5;21] na wengine walimuita mjinga,lakini alisamehe
yote. Je, mimi na wewe tuko tayari kuiga mfano wake? Abrahamu Lincoln raisi wa
16 wa Marekani alikuwa na wapinzani wengi waliokuwa wakimkosoa vibaya na
alipoulizwa ni kwanini hapendi kuwaadhibu hao madui zake, yeye alikuwa na haya
ya kusema juu ya hao wapizani wake ninawaangamiza maadui zangu kwa kuwasamehe
na kuwafanya marafiki
Samehe wengine
Bwana Yesu alitufundisha kupitia
kwa mtume Petro kusamehe saba mara sabini yaani kusamehe bila mipaka. Msamehe
jirani yako, msamahe mwenzi wako wa ndoa, msamehe mtawa mwenzako, wasamehe
marafiki zako, wasamehe viongozi wako na wasamehe ndugu zako pia, mfano mzuri
ni Yosefu wa agano la kale aliyeuzwa na ndugu zake utumwani,lakini alikuwa
tayari kusamehe na kuwasaidia hao ndugu zake licha ya kwamba walimtendea jambo
baya sana kibinadamu. Biblia inatuambia tafuteni kwa bidii kuwa na Amani na watu
wote na huo utakatifu hakuna mtu atakayemuona baba asipokuwa nao [Ebr 12:14]. Kusamehe wengine na kijsamehe mwenyewe ni
tiba tena ya magonjwa sugu. Nimewahi kumsikiliza Bwana mmoja aliyepona ugonjwa
wa moyo baada ya kukubali kumsamehe bosi wake aliyemdhulumu mshahara wake.
JINSI YA KUSAMEHE NA KUSAHAU
i.
Omba
neema ya Mungu kwa njia ya sala kwa sababu msamaha ni tendo la kiroho na wala
sio rahisi kulifanya kibinadamu
ii.
Kataa
kuongozwa na Hasira: muwe na hasira lakini msitende dhambi, Jua
lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka wala msipe ibilisi nafasi [Efe
4;26-27]
iii.
Tafuta
mtu mwenye busara anayeweza kuwa mshauri wako hasa katika nyakati ngumu zenye
ugumu wa kuachilia maumivu, unaweza ukawaona hata viongozi wako wa dini
iv.
Jenga
utamaduni wa kujishusha, uwe mnyenyekevu
v.
Usiweke
makwazo moyoni mwako, yakija yapokee kama kitu cha kawaida wala usipaniki
vi.
Tambua
madhara ya kutosamehe
vii.
Tamadunisha
maisha ya upendo
viii.
Tambua
usiposamehe nawe hautasamehewa na wala sala yako haitajibiwa
ix.
Tumia
msaada wa neno la Mungu [Biblia] mtume Paulo anasema neno la Mungu na likae kwa wingi
mioyoni mwenu [kolos 3;16]
x.
Uwe
mvumilivu, sio kitu kidogo tu unajaa uchungu moyoni
Tuombe
neema ya Mungu atujalie nguvu na uthabiti wa
kutoa na kupokea msamaha, ingawa ni kweli kabisa kuwa neno hili samehe
kwa tulio wengi ni neno gumu na zito kwa sababu tumejeruhiwa sana na wenzetu.
Ukiwa katika hali hiyo fungua moyo wako na ukamkaribishe Bwana YESU naye
atakusaidia.
MASHUJAA WALIOTOA MSAMAHA
Nelson
Mandela [1918-2013],
Hayati mzee Nelson Mandela alifungwa gerezanikwa miaka 27 bila kuwa na hatia
yoyote. Humo gerezani aliteswa na kupata manyanyaso ya kila aina toka kwa
makaburu. Lakini baada ya kuachwa huru na kutangazwa kuwa raisi naye akatangaza
msamaha kwa watesi wake ingawa alikuwa na uwezo wa kulipa kisasi. Baada ya
kutoka grezani alisamehe na kusema kuwa, Nilivyotembea kutoka mlangoni na kuelekea
lango ambalo nilikuwa natokea na kwenda kwenye uhuru wangu, nilijua kama
nisingeacha ukali wangu na chuki nyuma yangu, ningeendelea kuwa mfungwa.
Mandela aliwahi pia kusema kuwa, Watu wenye ujasiri hawaogopi kusamehe kwa
ajili ya Amani
Mt.
Papa Yohani Paulo II [1920-2005],
Huyu anajulikana pia kama mwanariadha wa Mungu kwa sababu ya bidii yake ya
kueneza injili ya Kristo Duniani, Siku ya tarehe 13 May 1981 Papa Yohani Paulo wa pili alipokuwa
akihutubia watu kwenye viunga vya Mt. Petro vatican alipigwa risasi kali ambazo
nusura zikatishe uhai wake, baada ya kukimbizwa hospitali kwa matibabu na
kupata nafuu alimsamehe kijana Mehmet Ali Agca aliyemfanyia hayo madhara na
alikwenda gerezani kumtembelea na kuzungumza nae.
Mt.
Josephina Bakhita [1869-1947],
Tunapenda kumuita mtumwa aliyekutana na kristoBakhita aliteswa sana utumwani na
kuachiwa alama za minyororo na makovu yapatayo 144 mwilini mwake baada ya
kukatwakatwa kwa kisu kikali na kisha vidonda vile vikapakwa chumvi. Hebu
fikiri Bakhita alipata uchungu na maumivu makali kiasi gani? Pamoja na maumivu yote
aliyopataBakhita alifungua moyo wake kwa Yesu Kristu na kutangaza msamaha kwa
watesi wake kwa maneno haya: nimewasamehe wote walionitesa utumwani na
kama ningekutana nao ningewabusu miguu, kwa sababu pasipo wao kunitesa kwa
mateso makali nisingemjua kristo.
Mashujaa
wengine ni kama Stephano [ Mdo 6;8-10,7;54-60 ] na Martin Luther King
[1929-1968], yeye pia aliwasamehe maadui zake waliokuwa wanapinga juhudi zake
za kutetea haki za wanyonge, alitufundisha kuwa Chuki haiwezi kuondoa chuki ni
upendo pekee unaoweza kufanya hivyona aliuawa kwa sababu ya chuki za
watu.
Hitimisho,Unaposoma au kusikia ujumbe huu
ni vema mimi na wewe tukajitafiti maisha yetu tuone ni wapi mahusiano yetu na
wenzetu yameharibika na kisha tuchukue hatua za kuanza mchakato wa kuleta Amani
na maridhiano.
Utambulisho
wa mkristo ni upendo na utambulisho wa upendo ni msamaha. Je, mimi na wewe tuko
tayari kutoa na kupokea msamaha?Papa Francis alitufundisha kuwa,msamaha
huleta furaha pale uchungu ulipoleta maumivu, huleta uponyaji pale uchungu
ulipoleta magonjwa..
Mungu
wetu ni mpole na mwenye huruma [Luka 1;78]
Tumsifu
Yesu kristu………………………
Imendaliwa
na:
Frt Peter Mwikwabe, wa Shirika
la Mateso ya Yesu kristu [wapasionisti]toka seminari kuu ya Falsafa ya Roho
mtakatifu-Arusha [Spiritan Missionary Seminary].
Makala
hii imeandaliwa kwa msaada wa vitabu vya You are not Rejected, Huruma ya Mungu ni kwa
watu wote, We are more than conquerors,Matatizo ni daraja, Biblia takatifu
na taarifa mbalimbali za mtandaoni.
0757724342
Email:
petermwikwabe20@gmail.com

Comments
Post a Comment