TANZIA: PADRI WA KWANZA MZALENDO WA SHIRIKA LA WAMISIONARI WA DAMU AZIZI YA YESU PROVINSI YA TANZANIA AZIKWA

Na Rodrick Minja, Manyoni.
Imeelezwa kuwa tunapaswa kujifunza kuwa uhai ni mali ya mungu na anaweza kuichukua siku na saa anayoipenda yeye mwenyewe.
 Hayo yameelezwa na Askofu Edward Mapunda wa jimbo Katoliki la Singida wakati wa ibada ya mazishi ya Padre wa kwanza mzalendo wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Provinsi ya Tanzania Padre Onesphory Kayombo, ibada iliyofanyika katika Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni Jimboni Singida.
Askofu Mapunda amesema kuwa kwa kutambua hilo hakuna sababu ya kumuuliza mwenyezi mungu ni lini na saa gani anaweza kuuchukua uhai wako bali unachopaswa ni kujiweka tayari kiroho na kimwili.
Amesema kuwa wakati huu wa kipindi cha kwaresma tunapaswa kujitafakari na hususani kutafakari maneno tuliyoambiwa siku ya jumatano ya majivu kuwa sisi tu mavumbi na mavumbi tutarudi.
Askofu Mapunda amesema kuwa kwa kutafakari maneno hayo tunapaswa kuwa watu wa kutenda haki kwani kwa kufanya hivyo ndiyo kiini cha dini ya kweli.
Aidha amewataka wamaini wote kuwatendea haki maskini ili tuwe  salama mikononi mwa mwenyezi mungu.
Akimzungumzia Marehemu Padre Kayombo Askofu Mapunda amesema kuwa Padre Kayombo alikuwa ni padre aliyeupenda wito wake, aliyeuthamini, aliyeuheshimu, aliyeufurahia na laiyekuwa mtu wa kuwashirikisha wengine zawadi ya wito aliyokirimiwa na mwenyezi mungu, hivyo tujifunze kutoka kwa yale mema aliyotuachia hapa duniani.
“Kwa kweli Marehemu Padre Onesphory Kayombo alikuwa ni Padre wa mfano na laikuwa kweli ni tunda la kwanza la Wamisionari wa damu Azizi ya Yesu Provinsi ya Tanzania kwa jinsi alivyouishi utume na wito wake” aliongeza Askofu Mapunda.
‘Mwaka Juzi yaani 2016 btulikuwa nae hapa Parokiani Manyoni pamoja na mwenzake Padre Felix Mushobozi wakati wakisherehekea Jubilei ya miaka 25 ya upadre wao leo hii hatunaye ,hivyo ninawaomba tuendelee kumshukuru mwenyezi mungu kwa yawadi ya uhai wake, wito wake wa upadre kwani wito huo ni zawadi aliyotiwa kwa sauti moja toka kwa mwenyezi mungu nay eye akaiitikiwa kwa moyo mmoja” Alisema Askofu Mapunda.
Askofu Mapunda akiendelea na homilia yake amesema kuwa mungu wetu ni wa haki na amani hivyo tunapaswa kuwa waaaminifu kwa mwenyezi mungu na  ili haki hiyo ionekane inatupasa tulinganishe matendo na mawazo yetu.
Hata hivyo aliwataka waamini kutenda haki kwani msingi wake ni yesu kristona anayempenda yesu kristo anakuwa ametenda haki.
“Kutenda haki ni kuwa walinzi na kujali binadamu wengine kwani baada ya maisha ya utume na wito wetu  hapa duniani tutakuwa pamoja na bwana wetu, na msingi wa matumaini hayo ni kuishi milele na yesu kristo mwenyewe huku tukitegemea msingi wa imani ya ufufuko.
Askofu Mapunda katika mahubiri yake pia ametolea mfano wa wanawali walioalikwa harusini ambapo wengine walikuwa na taa ambazo hazikuwa na mafuta na wengine walikuwa na taa zenye mafuta hali ambayo iliwapelekea wengine kushindwa kumlaki bwana harusi alipofika nyumbani.
Amesema kuwa wale wanawali waliokuwa na taa ambazo hazina mafuta watakuwa ni waamini wapumbavu na wale waliokuwa na taa zenye mafuta watakuwa ni waamini wenye busara.
“Mfano huu unatuonyesha ni wapi tunapoelekea na nini tunapaswa kukifanya  hivyo hakikisheni kuwa mnakesha kila wakati mkiwa katika hali ya usafi wa kiroho na kimwili na kila mmoja wetu atapaswa kuanza kuchagua kundi analotaka kuwepo iwe ni lile la wenye mafuta au wasiokuwa namafuta” aliongeza Askofu Mapunda.
Askofu amesema kuwa kifo huwa siku zote kinamkumbusha kila mmoja wetu kujinunulia mafuta na mafuta hayo ni kumrudia mwenyezi mungu hivyo tunapaswa kuwjiweka tayari kila wakati.
Aidha Askofu Mapunda amewataka waamini kuwa watu wenye kutenda matendo ya hurumakuwa walinzi wa wengine na kuwa watu wa majitoleo kwani kwa hivi sasa tunasikitika kwa sababu mwenzetu ametangulia mbele ya haki, hapa kinachotupasa ni kujipa faraja  kwani yesu kristo ametuahidia uzima wa milele.
Marehemu Padre Onesphory Lazaro Kayombo alizaliwa Septemba 08, 1960 katika kijiji cha Lupingu Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe , alipewa Daraja la Takatifu la ushemasi Januari 12, 1991 katika Parokia ya mtakatifu Gaspar Roma Italia na tarehe 29 Septemba 1991 alipewa daraja takatifu la Upadre na Hayati Mhashamu askofu Bernad Mabula wa Jimbo katoliki Singida katika Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni.
Kwa upande wake Mkuu wa Shirka la Wamisionari wa  Damu Azizi ya Yesu Provinsi ya Tanzania Padre Chesco Peter  Msaga akimuelezea Marehemu Onesphory Kayombo alisema kuwa wao kama Shirika wanamajonzi makubwa yakuondokewa na mwanahirika wao amabye alikuwa ni kiungo kikubwa baina yao na waamini mahalia hususani katika Parokia alizokuwa akifanya kazi na utume wake.
Padre Msaga katika kutoa salamu  za Shirika  Provinsi ya Tanzania amewashukuru wazazi wa Marehemu Padre Kayombo kwa majitoleo yao ya kumtoa mwanao katika shamba la bwana, ili atumike kutenda, pili amewashukuru waamini na waombolezaji wote walioshiriki kwa namna  yeyote ile katika kufanikisha maziko ya Padre Kayombo huku akisema kuwa pengo aliloliacha kamwe halitazibika.
“Ninakumbuka Mzee lazaro Kibiriti Kayombo ni mmojawapo wa wazee waliowapokea wanashirika wa kwanza hapa Manyoni mwaka 1966 waliokuwa wakiongozwa na Padre Dino Gioia na hata leo hii tunamkumbuka kwa yale yote aliyotukirimia na  hakuishia hapo aliona ni vyema kumtoa mwane naye atumike katika kanisa asante sana Mzee KayomboMungu akubariki” aliongeza Padre Chesco Msaga.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Ulimwenguni Padre walter Milando alisema kuwa Marehemu Padre Kayombo alikuwa ni mafano kwao kwani alikuwa ndiye tunda la kwanza  la wamisionari kufika hapa Tanzania hivyo alisema kuwa kazi tuliyopewa sasa ni kuhubiri injili ya mungu.
Padre Milando pia ametaka tutafakari ukristo wetu kwani kifo chake ni mbegu iliyopandwa na inatupa nguvu ya kwenda mbele kuendeleza upendo wa kristo.
Kwa upande wake Padre Anthony Marunda wa Jimbo Katoliki Moshi alisema kuwa yeye kama rafiki na zaidi ya ndugu alimfahamu Marehemu Kayombo wakati alipokuwa anasoma Kibosho Seminari akisomea masomo ya falsafa ndipo walipoanza safari ya undugu.
Padre Marunda alisema kuwa watenda kazi katika shamba la bwana ni wachache hivyo tuna kila sababau ya kuhuzunika kwani kupoteza kondoo mmoja ndani ya zizi ni vigumu kumrudisha kama yule  yule.
Alisema kwa kumuenzi marehemu Kayombo Onesphory ni kwa kuomba neema ya kuwa na nguvu na ujasiri na moyo wa kujituma pindi tunapokutana na misukosuko.
Padre Marunda alisema kuwa Marehemu Kayombo alikuwa ni mtu jasiri na alisimama katika ukweli ana daima alisimama imara katika utendaji kazi katika shamba la Bwana hivyo tuna kila sababu ya kulia na kuhuzunika kwani tumempoteza shujaa na mtu aliyejituma.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wananchi wa Manyoni Mbunge wa Manyoni Mashariki Bwana Daniel Mtuka alisema kuwa hatupaswi kuhuzunika kupita kiasi kwani tulizaliwa na siku moja tutaondoka kurudi kwa muumba wetu.
Alisema  katika maandiko matakatifu yanasema kuwa mtu akihuzunika sana haamini kama mbeleni kuna ufufuko hivyo tujue ya kuwa Marehemu Kayombo amelala na siku ya mwisho atafufuka kumlaki bwana mawinguni.
Alisema kuwa kazi ya kulea miito ni kazi kubwa sana, na ni kazi yenye kutumia gharama kubwa hivyo kwa sasa shambani mwa bwana mavuno ni mengi ila watendakazi ni wachache hivyo anapoondoka mmoja ni kazi kubwa sana kumpata mwingine.
Aidha aliwataka waamini mbalimbali kumuenzi kwa yale yote mema aliyoyafanya wakati wa uhai wake na pia kuendelea kumwombea ili pumzike kwa amani huko mbinguni.

Comments