Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania Tawi la Arusha Dr. Adelardus Kilangi ameapishwa wikii hii Bungeni Dodoma kuwa Mbunge baada ya Kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mbele ya Mheshimiwa Naibu Spika wa Bunge Dr. Tulia Atinkson Bungeni Dodoma Jumatatu, Mheshimiwa Dr. Adelardus ameahidi kuwa Mwaminifu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutenda majukum yake kama mwanasheria Mkuu wa serikali katika Misingi ya haki na usawa.
Awali wiki iliyopita Mhe. Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli alimteua Dk. Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hivyo kutoendelea na majukum yake kama Mkurugenzi wa SAUT Arusha.
Kabla ya Uteuzi huo, Mhe Dr. Kilangi alikuwa Mwenyekiti wa MAMLAKA YA UDHIBITI WA MKONDO WA JUU WA PETROLI NA GESI WA TAIFA kwa kuteuliwa na Raisi.
Kwa nyakati tofauti wahadhiri wa Chuo kikuu cha SAUT Mwanza na tawi la Arusha wamesema wamefurahishwa na Uteuzi wa raisi lakini wanasikitika kumpoteza Jalimu Nguri wa Sheria hasa katika Sheria za Madini na Sheria za kimataifa.
“Tumefurahi sana Dk. Kilangi kuteuliwa Mwanasheria Mkuu, lakini binafsi kwangu ni pigo kubwa kuanza kufikiria kumpata mtu atakayeendeleza mipango aliyoanzisha katika Tawi la Arusha” alisema Dr. Thadei Mkamwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tawi la Msimbazi Dr. Charles Kitima amemshukuru Dr. Kilangi kwa kukubali uteuzi wa Raisi kuwa amekipatia heshima Chuo cha Sauti.
Dr. Kitima amesema zipo Changamoto nyingi katika Sekta ya Sheria zinazohitaji mabadilik ili kuleta maendeleo na hivyo ana imani kuwa Dr. Kilangi atakuwa Mshauri mzuri wa Raisi.
Dr. Kilangi amefundisha Chuo cha Saut kwa zaidi ya miaka 10 kama Mhadhiri Msaidizi SAUT IRINGA (RUCO), Kisha Mhadhiri SAUT Mwanza na Mkuu wa Kitivo cha sheria na baadae akateuliwa na Balaza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuwa Mkurugenzi wa chuo cha Saut Arusha.
Kwa Upande wa Nje ya Nchi, Dr. Kilangi kwa muda Mrefu amekuwa Mjumbe na baadae Raisi katika Tume ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Afrika (AUCIL) na hadi sasa ni mtafiti wa sheria ya Umiliki rasilimali (Permenent Sovereignty over natural Resources) katika Nchi za Africa.
Dr. Kilangi alizaliwa Mkoani Geita na kusoma Shule ya Msingi Nyankumbu na Sekondari ya Sengerema (SESESCO) na Seminary za Nyegezi, Kibosho na Kipalapala na kisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia Shahada yakwanza hadi Uzamivu (PhD).

Comments
Post a Comment