ASKOFU MKUU DALLU AONYA..

ASKOFU MKUU wa Jimbo Kuu Katoliki SONGEA Mhashamu Damiani Denis Dallu amewataka Waamini, Mapadri pamoja na Watawa kuwa na hofu ya Kimungu katika kutimiza wajibu wao na majukumu ya kila siku.

Askofu Mkuu DALLU ametoa wito huo  katika mahubiri yake wakati wa Ibada Takatifu ya kubariki mafuta matakatifu ibada, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Kuu Katoliki SONGEA.

Amesema kuwa kukosekana kwa hofu ya Mungu kulipelekea wana wa ISRAELI kuingia utumwani Babeli, ambapo yalikuwa matokeo ya kumuasi Mungu, hivyo basi Mkristo yoyote yule anapaswa kuwa na hofu ya Mungu wala si hofu ya kiutawala kama waliyokuwa nayo wana wa ISRAEL.

Akizungumzia Mafuta Matakatifu, Askofu DALLU amesema tangu mwanzo kulikuwako na utaratibu wa kuweka Wakfu kwa kuwapaka mafuta watu kama walivyofanyiwa Watawala na manabii, ambapo amewataka Mapadri kuwa Watakatifu kama mafuta wanayoyabariki na kuyatumia katika Sakramenti za Kanisa.

Askofu DALLU amehitimisha mahubiri yake kwa kuwahimiza Mapadri wote kuzidisha juhudi katika kuchuchumilia Utakatifu  wakiwa na hofu  ya Mungu ndani mwao, ili wanapotumia mafuta hayo watu watakatifuzwe.

Comments