TUNU ZENU ZISIWAPE KIBURI-ASKOFU MKUU KINYAIYA AWAASA MAPADRI

Na Rodrick Minja, Dodoma

Waamini wa Kanisa Katoliki nchini wameaswa kufahamu kuwa mafuta Matakatifu ya  Krisma yalitokana na Utakatifu wa Kristo na hivyo kupewa jina hilo ili kuleta ukombozi kwa wale wote waliozaliwa mara ya pili.



Hayo yamebainishwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu   Beatus Kinyaiya wakati wa ibada ya misa takatifu ya kubariki mafuta ya krisma iliyofanyika  katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimboni hapa.



Askofu Mkuu Kinyaiya amesema kuwa katika maisha yetu tunapaswa kuwa watu wenye kutenda matendo ya huruma kwani Mwenyezi Mungu amefanya hivyo kwa upendo usio na kifani kwa ajili ya kutuandalia mkombozi ambaye aliteswa, akafa na hatimaye akafufuka siku ya tatu kwa ajili ya kutukomboa sisi wanadamu kutoka katika lindi la dhambi.



Hata hivyo amesema kuwa sisi ni wanadamu ambao ni wakosaji na wenye dhambi hivyo ni muhimu kujitafakari kwa kina na baada ya hapo tujue haya tunayoyafanya tunayafanya kwa nguvu za nani na hata kama ni sifa tunapewa tunapaswa kuzitafakari sifa hizo kama tunastahili kuzipokea.



“Alikuwepo Padri mmoja ambaye alikuwa ni muhubiri mzuri na hodari wa kutoa mahubiri yaliyo mema na mazuri kwa waamini lakini alikuwa mara baada ya ibada anatoka nje na kuanza kujisifia kwa waamini kuwa mmesikia vigongo nilivyotoa kwenye mahubiri?, sasa tujiulize tusisahau tunafanya kwa urahisi na kupata sifa nyingi je aliyetuwezesha tunamkumbuka?” aliongeza Askofu Mkuu Kinyaiya.



Kwa upande wa mapadri, Askofu mkuu Kinyaiya amewataka mapadri kutumia tunu, karama na vipaji walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu katika kulikuza shamba lake na siyo kinyume na hapo.



Askofu Mkuu Kinyaiya alisema kuwa wapo baadhi ya Mapadri wamekuwa wakitumia vipaji na tunu walizojaliwa kinyume na mapenzi ya mungu hivyo kuwataka kubadilika .



“ Tunu, karama na tunu mlizojaliwa zisiwape kiburi, Mwenyezi Mungu kawawezesha hivyo mshukuruni kwa kuwawezesha kwa yote mlionayo” aliongeza Askofu Mkuu Kinyaiya.



Pia amewataka kutokukubali kuruhusu kishawishi chochote kile amabacho kitawapelekea kukengeuka na kuanguka katika njia yao iliyo nzuri na badala yake kuwataka kusimama kidete katika kulihubiri neno la Mungu na katika utume wao.



Kuhusiana na wito waliouchagua, Askofu Mkuu Kinyaiya amewataka kujenga upendo baina yao kama bwana wetu Yesu Kristo alivyosema kuwa amri kuu nawapeni ni upendo Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.



Hata hivyo amewataka mapadri kuhakikisha wanapokutana katika dekania zao wajenge kasumba ya kuendesha ibada ya misa kabla ya mikutano yao na kuwataka mapadri wote wanaofanya kazi za utume katika Jimbo kuu Katoliki Dodoma kuhudhuria mikutano hiyo kwani mikutano hiyo ya dekania sio maalumu kwa mapadri wa Dekania pekee bali ni kwa mapadri wote waliopo katika Jimbo Mahalia.



Askofu Mkuu Kinyaiya pia amezitaka Parokia Dada kukaa na kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kusaidiana ili kusongesha mbele gurudumu la utume katika Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.



Askofu Mkuu Kinyaiya amesema kuwa mapadreiwana wajibu wa kushirikiana katika kila jambo na kuweka mbali tofauti zao za kidekania ili kuweza kusimamia vyema kondoo zao na hatimaye kujenga mahusiano mazuri baina yao na waamini wao kwa kutengeneza mazingira ya kutembeleana hata katika vituo vyao wanavyofanyia utume.



Kuhusu utoaji wa Sakramenti ya Kitubio amewashauri mapadri kuwa wanabadilishana wa parokia hii anakwenda parokia ya mwenzake kwa ajili ya kutoa sakrtamenti ya kitubio kwani wengi wa waamini wanashindwa kushiriki sakramenti hiyo kutokana na mazoea na ukaribu au kumfahamu anayemuungamisha .



Katika ibada hiyo ya kubariki mafuta ya Krisma pia mapadri wamerejea viapo vyao vya utii kwa Askofu  mbele ya Baba Askofu mkuu na mbele ya waamini wote waliohudhuria katika ibada  ya misa takatifu.



Hata hivyo, Askofu Mkuu Kinyaiya amehitimisha kwa kuwapongeza waamini kwa utulivu wao katika parokia walizopo na pia amewataka mapadri kuhakikisha kuwa wanazitafutia suluhu ndoa zenye migogoro na changamoto mbalimbali.



Aidha Mafuta yaliyobarikiwa leo hii ni pamoja na Mafuta ya krisma ambayo hutumika kutabaruku Kanisa, Altare, kumweka wakfu Padri na Askofu, huku mafuta ya wakatekumeni yakitumika katika kuwabatiza wakatekumeni na mafuta ya wagonjwa yakitumika kuwapaka ili kuwapa  faraja.

Comments