VIJANA WAMUUNGE MKONO RAIS MAGUFULI-PAROKO

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Padri Onesmo Wissi amesema kuwa ni dhahiri kuwa vijana wamekomaa kiroho na kiimani hivyo wanapaswa kujitafakari kwa kina yale yote wanayoyatenda katika maisha yao ya kila siku.
Hayo ameyabainisha hivi karibuni wakati wa mahubiri yake ya Jumapili ya Matawi, ibada iliyofanyika katika Kanisa hilo na kuhudhuriwa na waamini mbalimbali.
Padri Wissi amesema kuwa kwa sasa kuna nafasi mbalimbali ambazo vijana wanaweza kuzitumia katika kujikwamua na janga la ukosefu wa ajira hivyo wanapaswa kuzichangamkia nafasi hizo.
Amesema kwa sasa wanapaswa kuunga mkono juhudi za Rais John Pombe Magufuli za Tanzania ya viwanda kwa kujikita zaidi katika kuangalia ni fursa gani ambazo zitasaidia kusukuma mbele maendeleo ya nchi yao.
Amewataka pia vijana kujiunga katika vikundi vya uazalishaji ili kuweza kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango ili kuweza kuziuza kwenye viwanda vitakavyoanzishwa hapa nchini.
Hata hivyo Padri Wissi amewashauri vijana kufanya tafiti kwa upande wa malighafi ambazo watazalisha ili ziwe na tija  katika viwanda na siyo kuzalisha bidhaa ambazo zitakosa hata soko katika viwanda vinavyoanzishwa.
Akihitimisha mahubiri yake Padri Wissi amewataka vijana kujiajiri na siyo kusubiri kuajiriwa kwani fusra za ajira zipo nyingi na endapo watachukua nafasi ya kuzichangamkia na hususani katika kujiunga na vikundi mbalimbali vya uzalishaji.

Comments